Nusu fainali ya pili ya Kombe la Dunia itasakatwa uwanjani Atlanta, Marekani leo Jumatano saa nne usiku kati ya Uingereza na mabingwa watetezi Argentina.
Uingereza inayoongozwa na Harry Kane inalenga kufuzu kwa fainali ya kwanza baada ya miaka 60, huku Argentina wakiwania kufuzu kwa fainali na kutetea kombe lao.
Itakuwa mara 6 kwa Uingereza na Argentina kukabiliana katika mechi za kimataifa, Uingereza wakishinda mechi 3, Argentina wakishinda mbili.
Uingereza waliibwaga Argentina mabao 3-1 mwaka 1962, kabla ya kuilaza Argentina bao moja bila mwaka 1966 katika robo fainali ya Kombe la Dunia.
Hata hivyo, Argentina pia walilipiza kisasi wakiishinda Uingereza mabao 2-1, katika robo fainali ya Kombe la Dunia.
Argentina walisajili ushindi wa mabao 4-3 kupitia penalti kwenye raundi ya 16 katika Kombe la Dunia mwaka 1998.
Uingereza iliwalemea Argentina mwaka 2002 walipokutana katika mechi ya makundi ya Kombe la Dunia.
Kuelekea nusu fainali ya leo, Argentina waliongoza kundi J wakizoa alama 9 kabla ya kuibandua Cape Verde 3- katika muda wa ziada kwenye raundi ya 32 bora.
Katika awamu ya 16 bora, Argentina chini ya kocha Lionel Scaloni iliwazidia maarifa Misri 3-2, na hatimaye kuilaza Uswizi 3-1, katika muda wa ziada katika robo fainali.
Uingereza yake Thomas Tuchel iliongoza kundi L kwa pointi 7, wakishinda mechi mbili na kutoka sare kabla ya kuishinda DR Congo 2-1, katika awamu ya 32 bora.
Three Lions iliwatimua wenyeji wenza Mexico 3-2 katika raundi ya 16, na hatimaye kuibwaga Norway 2-1, kupitia muda wa ziada.
Mshindi wa nusu fainali hiyo atakumbana na Uhispania katika fainali Jumapili hii mjini New York.