Mahakama Kuu ya Tanzania imetangaza kwamba zuio la serikali la matumizi ya mtandao wa kijamii wa X nchini humo ni kinyume na Katiba.
Imeamuru mamlaka husika kurejesha huduma hiyo mara moja bila vikwazo.
Jopo la majaji watatu katika Mahakama Kuu, Masjala Ndogo ya Dar es Salaam, liliamua kwamba kuzuia matumizi ya X tangu Mei 20, 2025, kunakiuka haki za kikatiba za uhuru wa kujieleza, kupata taarifa na kufuata taratibu za kisheria, kama zinavyolindwa na Katiba ya Tanzania ya mwaka 1977.
Mahakama imeagiza mamlaka kuondoa bila kuchelewa vizuizi vyote, kama kupunguza kasi ya mtandao na masharti mengine yaliyowekwa dhidi ya jukwaa hilo.
Kesi hiyo ya kikatiba iliwasilishwa na wanaharakati Tito Magoti na Kumbusho Dawson kwa niaba ya watumiaji wa X nchini Tanzania.
Majaji walibaini kuwa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania, TCRA, haikuwa na mamlaka ya kisheria ya kuzuia jukwaa zima, wakieleza kuwa sheria zilizopo zinalenga maudhui yanayokiuka sheria badala ya kufungia huduma nzima.
Pia, mahakama ilikosoa serikali kwa kutowapa watumiaji taarifa ya awali wala nafasi ya kupinga zuio hilo.
Serikali ilikuwa imetetea hatua hiyo iliyochukuliwa baada ya akaunti ya Jeshi la Polisi Tanzania kwenye X kudukuliwa, ikisema ililenga kulinda usalama wa umma na mifumo ya kidijitali.
Mahakama imefafanua kuwa mamlaka bado zina haki ya kuzuia au kuondoa maudhui yanayokiuka sheria.