Rais wa Ujerumani Dkt. Frank-Walter Steinmeier, amewasili Jijini Nairobi kwa ziara rasmi inayolenga kuimarisha ushirikiano kati ya nchi hizi mbili.
Alipowasili, Rais huyo alilakiwa na Mkuu wa Mawaziri aliye pia Waziri wa Mambo ya Nje Musalia Mudavadi.
Steinmeier akiwa ameandamana na ujumbe wa wafanyabiashara, anatarajiwa kushiriki mkutano wa pande mbili na mwenyeji wake Rais William Ruto, wakilenga kupanua biashara na uwekezaji, kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi na kuchochea maendeleo ya pamoja.
Ratiba ya Rais huyo nchini Kenya pia itajumuisha ziara kwenye miradi ya Ujerumani inayotekelezwa kwa pamoja na Kenya katika sekta ya afya, huduma za dijitali, ukuaji wa ujuzi, sanaa na utamaduni, akiangazia athari za ushirikiano huo.
Aidha, ziara hiyo inatoa fursa mwafaka kwa Kemya kuinua uchumi wake, kuvutia uwekezaji, kubuni nafasi za ajira na kuimarisha sekta za ushirikiano kwa manufaa ya nchi hizo mbili.