Bunge lataka polisi zaidi na barabara Meru, Isiolo

Hatua hii inalenga kukabiliana na wizi wa mifugo katika kaunti za Isiolo, Meru na maeneo jirani.

Marion Bosire
2 Min Read
Gabriel Tongoyo, Mwenyekiti Kamati ya Bunge Kuhusu Utawala na Usalama wa Ndani

Bunge linataka maafisa wa usalama waongezwe, barabara ziboreshwe na upatikanaji wa maji na malisho uimarishwe ili kukabiliana na wizi wa mifugo katika kaunti za Isiolo, Meru na maeneo jirani.

Mapendekezo hayo yametolewa na kamati za Bunge la Kitaifa zinazoshughulikia Utawala wa Kitaifa na Usalama wa Ndani, pamoja na Mshikamano na Fursa Sawa.

Hii ni baada ya wanachama kufanya ziara ya kutafuta ukweli kuhusu hali ya usalama katika Kaunti ya Isiolo.

Kamati hizo zilishauriana na maafisa wa usalama, viongozi wa kaunti, wazee na wakazi kufuatia ombi lililowasilishwa Bungeni na jamii za Isiolo na Meru kuhusu mashambulizi ya mara kwa mara, wizi wa mifugo na mgawanyo wa rasilimali za usalama.

Mwenyekiti wa kamati hizo Gabriel Tongoyo, alisema wamebaini changamoto kadhaa zinazohitaji hatua za haraka za serikali.

Mapendekezo ni pamoja na kuongeza idadi ya maafisa wa polisi, kujenga vituo zaidi vya polisi na vituo vya doria, kuongeza idadi ya Walinzi wa Kitaifa wa Akiba na kufungua barabara za kiusalama ili kurahisisha operesheni katika maeneo ya mbali.

Wabunge hao pia wametaka mipaka kati ya jamii zinazozozana ibainishwe na uwekezaji uongezwe katika barabara, mawasiliano, maji na elimu ili kukabiliana na ushindani wa rasilimali.

Tongoyo alisema kamati hizo zitaandaa ripoti ya uchunguzi wao pamoja na mapendekezo, ambayo yatawasilishwa Bungeni kwa ajili ya kujadiliwa na kuchukuliwa hatua.

Alisisitiza umuhimu wa ushirikiano akisema: “Tumejitolea kufanya kila linalowezekana kuwasaidia watu wa Isiolo, Meru na eneo lote kufikia amani na kukomesha kabisa ujambazi wa mifugo.”

Share This Article