Maseneta wa Kenya wameonya kuhusu ufadhili wa kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi unaotolewa kwa nchi za Afrika kupitia mikopo ya gharama kubwa badala ya misaada.
Kulingana nao, mikopo hiyo inazidisha mzigo wa madeni kwa mataifa ambayo tayari yanakabiliwa na majanga ya hali ya hewa.
Akizungumza katika mkutano wa COP31 mjini Antalya, Uturuki, Alhamisi, Novemba 19, Seneta wa Homa Bay Moses Kajwang’ alisema mafuriko na ukame vinavyokumba Kenya mara kwa mara husababisha hasara inayokadiriwa kuwa asilimia tano ya Pato la Taifa kila vinapotokea.
Alisema majanga hayo, ambayo awali yalikuwa yakitokea baada ya miongo kadhaa, sasa yanajirudia mara nyingi zaidi na kulazimisha serikali kukopa fedha kwa ajili ya kurejesha huduma na miundombinu.
Seneta wa Tana River Danson Mungatana alizitaka nchi za Afrika kuungana kudai ufadhili wa tabianchi wenye masharti nafuu, hususan mikopo yenye riba ndogo na misaada isiyohitaji kurejeshwa.
Alipendekeza pia kuanzishwa kwa taasisi ya Afrika ya kutathmini viwango vya mikopo ili kupunguza athari za tathmini za kimataifa zinazofanya nchi za Afrika kukopa kwa gharama kubwa.
Mungatana alionya kuwa kupanda kwa kina cha bahari tayari kunaharibu maisha ya wakazi wa pwani ya Tana River, akitaja hoteli moja ya Kipini iliyomezwa na bahari.
Ujumbe wa Kenya pia ulitaka kuimarishwa kwa usimamizi wa bunge kuhusu malengo ya kupunguza hewa ya methane na kuchunguza mifumo ya ufadhili wa nishati safi na ulinzi wa maeneo ya pwani.