Serikali yaangazia hatua za ziada kukabiliana na pombe haramu na mihadarati

Martin Mwanje
1 Min Read

Naibu Rais Prof. Kithure Kindiki leo Jumatano asubuhi aliongoza mkutano wa ngazi ya juu uliozileta pamoja asasi mbalimbali za serikali kwa lengo la kuangazia hatua zilizopigwa na namna ya kuimarisha vita dhidi ya pombe haramu na mihadarati.

Mkutano huo uliwaleta pamoja Makatibu, wakuu wa asasi za serikali na wadau wengine.

Mkutano huo ulitathmini utekelezaji wa maazimio ya awali na kukubaliana juu ya hatua za ziada za kushughulikia utengenezaji, usambazaji na uuzaji wa pombe haramu na mihadarati.

Masuala yaliyopewa kipaumbele yanajumuisha operesheni zinazofanywa kwa kujikita kwa ujasusi, kuweka udhibiti mkali kwa uagizaji na usambazaji wa dawa aina ya Ethanol, na ukaguzi mpya wa maeneo ya utengenezaji pombe miongoni mwa masuala mengine.

Mkutano huo pia ulisisitiza umuhimu wa hatua zilizoratibiwa, uwajibikaji mkubwa wa kitaasisi na ushirikiano endelevu kati ya serikali kuu, serikali za kaunti, asasi za udhibiti na jamii katika kulinda afya ya umma, usalama wa taifa na ustawi wa familia.

Share This Article