Waziri wa Usalama wa Taifa Kipchumba Murkomen, ameshiriki mazungumzo na mwenzake wa Italia Matteo Piantedosi, Jijini Rome, huku wakitia saini makubaliano ya ushirikiano katika sekta ya usalama baina ya nchi hizo mbili.
Makubaliano hayo yamebuni mkakati wa kuimarisha ushirikiano kati ya Kenya na Italia katika sekta za usalama, uhamiaji na utekelezaji wa sheria, hatua inayoimarisha ushirikiano wa muda mrefu kati ya nchi hizo mbili.
Kulingana na Murkomen, mazungumzo hayo yalielezea umuhimu wa kuimarisha ushirikiano katika kukabiliana na ugaidi na ufadhili wake, uhalifu wa kimataifa wa kupangwa, ulanguzi wa mihadarati na binadamu, uhalifu wa mtandaoni, usalama wa baharini na maswala ibuka ambayo yanahatarisha usalama.
Aidha, Murkomen alisema ushirikiano huo pia utabuni fursa za ubadilishanaji wa habari za kijasusi, mafunzo ya kitaaluma, usaidizi wa kiufundi, na utumizi wa teknolojia kukabiliana na changamoto za kiusalama.
“Ushirikiano wetu umejikita katika kuheshimu uhuru wa nchi, uzingatiaji katiba, sheria na haki za binadamu,” alisema Murkomen.
Murkomen, alisisitiza kuwa Kenya inadhamini urafiki wake na Italia na imejitolea kufanikisha uhusiano unaoimarisha usalama wa taifa, ulinzi wa wananchi na unaochangia amani na udhabiti wa kikanda na kimataifa.
Kwenye ziara hiyo nchini Italia, Murkomen ameandamana na balozi Fredrick Matwang’a, Naibu Inspekta Jenerali wa polisi Gilbert Masengeli, na maafisa wengine kutoka wizara ya Usalama wa Taifa.