Rais William Ruto leo Jumatatu analiongoza taifa kuadhimisha sherehe za 63 za Sikukuu ya Madaraka.
Ruto tayari amewasili katika Uwanja wa Wajir, kaunti ya Wajir kunakoandaliwa sherehe hizo.
Hii ni mara ya kwanza kwa sherehe hizo kuandaliwa katika kaunti hiyo, tangu kugatuliwa kwake.
Wakazi wenye hamu ya kushuhudia sherehe hizo zikiandaliwa eneo lao walifika uwanjani hapo asubuhi na mapema kujionea kwa mboni za macho yao namna zinavyoendeshwa.
Naibu Rais Prof. Kithure Kindiki, Maspika Moses Wetang’ula na Amason Kingi na Mawaziri mbalimbali ni miongoni mwa viongozi wanaotarajiwa kuhudhuria.
Aidha, Gavana wa Wahir Ahmed Abdullahi ambaye pia ni mwenyekiti wa Baraza la Magavana atawaongoza viongozi wengine wa eneo hilo kuhudhuria sherehe hizo.
Maafisa wa usalama wameshika doria eneo hilo kwa lengo la kuhakikisha sherehe hizo zinaendeshwa bila hata chembe ya nuksi.
Kwenye hotuba yake, miongoni mwa masuala mengine, Rais Ruto anatarajiwa kuangazia masuala mbalimbali yanayolikumba taifa, ikiwa ni pamoja bei za juu za mafuta ambazo zimekuwa kikwazo kwa wengi.
Aidha, huenda akazungumzia hatua zinazochukuliwa na utawala wake kuhakikisha usalama wa wanafunzi hasa katika shule za malazi.
Hii ni kutokana na moto ulioangamiza wanafunzi katika shule ya Utumishi Girls Academy mjini Gilgil, kaunti ya Nakuru Alhamisi wiki iliyopita.
Wanafunzi 16 waliangamia na 79 kujeruhiwa kwenye mkasa huo.