Bahati asimulia alivyomuasili Morgan

Alikutana naye katika kituo cha watoto yatima cha ABC jijini Nairobi zaidi ya miaka 15 iliyopita.

Marion Bosire
2 Min Read

Msanii wa muziki nchini Kenya, Kevin Bahati Kioko, maarufu kwa jina lake moja Bahati, amesimulia safari ya kuasili mwanawe wa kwanza Morgan.

Amegusa hisia za wengi akielezea alivyomchukua Morgan Bahati Kioko, aliyekutana naye katika kituo cha watoto yatima cha ABC jijini Nairobi zaidi ya miaka 15 iliyopita.

Kupitia ujumbe kwenye mitandao ya kijamii, Bahati alifichua kuwa Morgan aliokolewa kutoka mitaa ya Mathare na wafanyakazi wa kituo hicho, ambacho pia kilimlea na kumsaidia kupata elimu alipokuwa mdogo.

Msanii huyo alisema alikutana na Morgan wakati wa ziara zake katika kituo hicho baada ya kuanza kupata mafanikio katika muziki kufuatia kutamba kwa wimbo wake “Mama”.

Bahati, ambaye wakati huo alikuwa na umri wa takriban miaka 20, hakuwa ameoa na alikuwa akikabiliwa na changamoto za kifedha.

Hata hivyo, aliamua kumchukua mtoto huyo na kuwajibika kumlea huku akiendeleza safari yake ya muziki.

Alikumbuka ugumu wa malezi, akisema alilazimika kutekeleza majukumu ya baba, mama, mlezi na mpishi kwa wakati mmoja, huku wakati mwingine wakikumbana na changamoto hata za kupata chakula kilichoiva.

Kwa sasa, Morgan anatumia jina la Morgan Bahati Kioko na anasoma katika Shule ya Kitaifa ya Lenana.

Bahati amefurahikia maendeleo ya Morgan, akimtaja kuwa kijana mwenye akili na ufasaha wa kuzungumza, akimtambulisha kama mwanawe wa kwanza katika familia yake na mkewe, Diana Marua.

Share This Article