Mahakama ya Upeo yaimarisha maandalizi kushughulikia kesi za uchaguzi

Majaji wa mahakama hiyo wamekamilisha mafunzo ya siku mbili kuhusu usimamizi na uamuzi wa kesi za kupinga matokeo ya uchaguzi wa urais.

Marion Bosire
2 Min Read

Mahakama ya Upeo nchini Kenya imeimarisha maandalizi yake kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2027.

Majaji wa mahakama hiyo wamekamilisha mafunzo ya siku mbili kuhusu usimamizi na uamuzi wa kesi za kupinga matokeo ya uchaguzi wa urais.

Mafunzo hayo yaliyofanyika Novemba 9 hadi 10, 2026, yalijikita katika ushahidi wa uchaguzi, uchunguzi na kuhesabu upya kura, usimamizi wa kesi, masuala mapya ya kisheria, teknolojia ya uchaguzi, akili mnemba na taarifa potovu.

Yaliandaliwa na Kamati ya Mahakama kuhusu Uchaguzi, JCE, inayoongozwa na Jaji Mohamed Abdullahi Warsame, kwa ushirikiano na Chuo cha Mafunzo cha Mahakama ya Kenya, KJA.

Akifungua mafunzo hayo, Jaji Mkuu na Rais wa Mahakama ya Juu, Martha Koome, alisisitiza umuhimu wa kutumia uzoefu na maamuzi ya awali ya mahakama kuhusu chaguzi za mwaka 2013, 2017 na 2022, huku wakijiandaa kukabiliana na changamoto mpya zinazoweza kujitokeza mwaka 2027.

Mafunzo hayo ni sehemu ya mpango endelevu wa kujenga uwezo kwa watumishi wa Idara ya Mahakama, wakiwemo majaji, maafisa wa mahakama, makarani na wafanyakazi wengine wanaohusika na utatuzi wa migogoro ya uchaguzi katika mahakama na mabaraza mbalimbali.

Kupitia mpango huo, Idara ya Mahakama inalenga kuimarisha uwezo wake wa kutatua migogoro ya uchaguzi kwa uhuru, haki na haraka, kwa kuzingatia Katiba na sheria za nchi.

Mahakama imesisitiza kuwa haki katika masuala ya uchaguzi huanza na maandalizi madhubuti ya taasisi zinazohusika.

Share This Article