Mgonjwa wa mwisho wa Ebola aondoka hospitalini

Watu 11 waliokuwa kwenye karantini pia wameruhusiwa kwenda nyumbani wakiwa katika hali nzuri ya afya baada ya kubainika kutoambukizwa ugonjwa huo.

Martin Mwanje
1 Min Read

Mgonjwa wa mwisho wa ugonjwa wa Ebola ambaye amekuwa akipokea matibabu nchini ameruhusiwa kuondoka hospitalini. 

Hii ni baada ya mgonjwa huyo kupimwa na kubainika kutokuwa na ugonjwa huo.

Akiwahutubia wanahabari leo Jumatano, Waziri wa Afya Aden Duale amesema watu 11 waliokuwa kwenye karantini pia wameruhusiwa kurejea nyumbani wakiwa katika hali nzuri ya afya.

Hii ina maana kwamba Kenya kwa sasa haina mgonjwa yeyote wa Ebola wala hakuna mtu yeyote aliyewekwa kwenye karantini.

Katika kipindi cha siku 42 zijazo kuanzia kesho Alhamisi, Kenya itatangazwa kuwa isiyokuwa na ugonjwa wa Ebola ikiwa hakuna kisa chochote cha ugonjwa huo kitaripotiwa humu nchini.

Awali, Kenya iliripoti visa 9 vya ugonjwa wa Ebola huku wagonjwa wawili wakifariki kutokana na makali ya ugonjwa huo.

Wagonjwa 6 waliruhusiwa kwenda nyumbani baada ya kuthibitishwa kupona ugonjwa huo.

Wengi watatazamia kwamba hakuna kisa chochote cha ugonjwa wa Ebola kitaripotiwa nchini katika kipindi cha siku 42 zijazo.

Ikiwa hilo litajiri, basi Kenya itatangazwa kuwa nchi isiyokuwa na ugonjwa wa Ebola.

Share This Article