Malaika Gray afurahia mapokezi ya wimbo wake

Wimbo huo umetazamwa zaidi ya mara milioni mbili kwenye YouTube ndani ya siku 11 tangu ulipotolewa.

Marion Bosire
2 Min Read

Msanii chipukizi wa muziki nchini Tanzania Malaika Gray, amefurahia na kusherehekea mafanikio ya wimbo wake wa kwanza, ‘My Fever’, aliomshirikisha staa wa Bongo Flava, Marioo.

Haya yanajiri baada ya wimbo huo, kutazamwa zaidi ya mara milioni mbili kwenye jukwaa la mtandaoni la YouTube ndani ya siku 11 tangu ulipotolewa.

Kupitia ukurasa wake wa Instagram, Malaika aliwashukuru mashabiki kwa upendo na sapoti kubwa, akieleza kuwa mafanikio hayo yametimiza moja ya ndoto zake kubwa katika muziki.

“Views milioni mbili ndani ya siku 11 tu, hata wiki mbili hazijafika. Asanteni sana kwa upendo, sapoti na kuendelea kusikiliza My Fever,” aliandika.

Malaika alizaliwa mwaka 2006 jijini Brisbane, nchini Australia, akiwa na mama Mtanzania na baba mwenye asili ya New Zealand.

Mwaka 2012, alihamia Johannesburg, Afrika Kusini, ambako alianza kukuza kipaji chake cha muziki na kuimba akiwa na umri wa miaka sita.

Msanii huyo anayechipukia katika mitindo ya Afropop, R&B na Pop kwa sasa anasomea uimbaji na biashara ya muziki katika Chuo cha Berklee College of Music kilichopo Boston, Massachusetts, Marekani.

Wimbo wa ‘My Fever’ ulitolewa Oktoba 30, 2026, ukiwa mwanzo wa safari yake rasmi katika tasnia ya muziki.

Malaika aligharamia utayarishaji wa wimbo huo kwa kujitegemea na anamiliki haki za rekodi zake za muziki, huku akichanganya ladha za muziki wa Afrika Mashariki na mitindo ya kisasa.

Share This Article