Shirika la Afya Duniani, WHO limeipa Kenya vifaa tiba vya kukabiliana na virusi vya Bundibugyo vinavyosababisha ugonjwa Ebola.
Ujumbe wa WHO ukiongozwa na Mkurugenzi wa Kikanda wa bara la Afrika, Prof. Yakub Janabi ulimkabidhi Waziri wa Afya Aden Duale vifaa hivyo ulipomtembelea na kufanya mazungumzo naye afisini mwake leo Jumatatu.
Wakati wa mazungumzo hayo, hatua zilizowekwa na Kenya katika kukabiliana na ugonjwa wa Ebola ziliangaziwa.
Vifaa tiba vilivyokabidhiwa Waziri Duale vinajumuisha msaada wa kiufundi na utendaji kazi, ikiwa ni pamoja na bidhaa muhimu za kukabiliana na ugonjwa huo na vifaa vya kutumiwa na wahudumu wa afya kujikinga.
WHO pia ikielezea kuridhishwa na Taratibu za Utendaji Kazi za Viwango vya Uangalizi za Filovirus.
Kenya haijaripoti kisa chochote cha ugonjwa huo katika kipindi cha wiki tatu zilizopita.
Hata hivyo, hadi sasa imeripoti visa 9 vya ugonjwa wa Ebola huku wagonjwa wawili wakifariki kutokana na makali ya ugonjwa huo.
Kwa upande mwingine, wagonjwa 6 wamepona ugonjwa huo na kuruhusiwa kwenda nyumbani wakati mmoja akiendelea kupokea matibabu.
Wasafiri zaidi ya 772,000 wamepimwa katika maeneo 28 ya kuingia nchini huku sampuli 736 zikipimwa katika maabara tano zilizotengwa.
Duale amesisitiza umuhimu wa kuendelea kuwa macho kupitia uangalizi kamili, uchunguzi wa haraka na kuendelea kuchukua vipimo katika maeneo ya kuingia nchini.