Wanariadha wa Kenya Abigael Kosgei na Enock Tuitoek, walishinda dhahabu Jumapili jioni huku riadha ikianza katika michezo ya Olimpiki kwa chipukizi mjini Dakar, Senegal.
Kosgei alinyakua dhahabu ya mbio za mita 2,000 kuruka viunzi na kidimbwi cha maji kwa kutumia dakika sita sekunde 30.24.
Tsedikan Mekonen wa Ethiopia alishinda fedha huku Elif Celik wa Uturuki akiridhia shaba.
Kenya pia ilijiongezea dhahabu nyingine baada ya Enock Tuitoek kushinda mbio za mita 3,000, alipotimka kwa muda wa dakika 8 sekunde 7.69.

Goytom Mekonen wa Ethiopia na Mezziane Benhammou wa Ufaransa walishinda medali za fedha na shaba mtawalia.
Kenya inashikilia nafasi ya tisa katika msimamo wa nishani kufikia sasa kwa dhahabu 3.
China inaongoza kwa medali 17 (dhahabu 11, fedha 4, shabaa 2) ikifuatwa na Japani kwa medali 16 (dhahabu 9 fedha 3 na shaba 4) nayo Urusi ni ya tatu kwa nishani 10 (dhahabu 6 na fedha 4).