Mawakili wa Mwenyekiti wa chama cha upinzani nchini Tanzania CHADEMA, Tundu Lissu, wameanza rasmi mchakato wa kupinga hukumu ya kifungo cha miaka minne jela iliyotolewa dhidi yake kwa kosa la uchochezi.
Wakili wake, Paul Kisabo, amesema kundi la utetezi tayari limewasilisha taarifa ya nia ya kukata rufaa katika Mahakama ya Rufaa, likisubiri kupata nyaraka za hukumu na mwenendo wa kesi ili kuandaa hoja za kisheria.
Akizungumza jana Jumapili Novemba 8, 2026, Kisabo alisema taarifa hiyo iliwasilishwa na Mwanasheria Mkuu wa CHADEMA, Dkt. Rugemeleza Nshala, Novemba 6, ndani ya muda unaotakiwa kisheria.
Amesema utetezi unapinga uamuzi wa Mahakama kumtia Lissu hatiani kwa uchochezi, akieleza kuwa shtaka hilo halikuwa sehemu ya mashtaka aliyokabiliwa nayo wala utetezi alioutoa mahakamani.
Aidha, mawakili wanahoji uamuzi wa kumpa kifungo cha miaka minne badala ya faini, wakitaja kifungu cha 35 cha Kanuni za Adhabu kama msingi wa hoja zao.
Lissu alihukumiwa Novemba 6, 2026, na Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo ya Dar es Salaam, baada ya kuachiwa huru kwenye shtaka la uhaini.
Kesi hiyo ilidumu takribani miezi 19 tangu alipokamatwa Aprili 9, 2025, mjini Mbinga, Ruvuma, kufuatia kuhutubia mkutano wa CHADEMA.
Alikuwa akiendeleza kampeni ya kuhimiza mabadiliko ya kanuni za uchaguzi kabla ya uchaguzi mkuu wa mwaka jana.