Amnesty International yalalamikia hukumu ya Lissu

Kulingana na shirika hilo, hukumu hiyo ni ukiukaji mkubwa wa haki na matokeo ya kesi iliyokosa misingi ya haki.

Marion Bosire
2 Min Read
Tundu Lissu, Kiongozi CHADEMA

Shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International, limelalamikia hukumu ya kifungo cha miaka minne gerezani iliyotolewa dhidi ya Tundu Lissu.

Kulingana na shirika hilo, hukumu hiyo ni ukiukaji mkubwa wa haki na matokeo ya kesi iliyokosa misingi ya haki.

Katika taarifa, Mkurugenzi wa Kanda ya Afrika Mashariki na Kusini wa shirika hilo, Tigere Chagutah, alisema hukumu dhidi ya Lissu ilitokana na mchakato usio wa haki uliokiuka haki zake za msingi.

Chagutah alibainisha kuwa Lissu alikuwa amekaa gerezani kwa siku 577 bila dhamana, huku akinyimwa nafasi ya kuwasiliana kwa faragha na mawakili wake, hali iliyomlazimu kujitetea kwa kiasi kikubwa.

Pia alielezea wasiwasi kuhusu kukatizwa kwa matangazo ya moja kwa moja ya kesi, madai ya kuteswa na kufukuzwa nchini kwa waangalizi wa kimataifa wa kesi hiyo, pamoja na mazingira yasiyo ya kibinadamu aliyozuiliwa.

Amnesty International imezitaka mamlaka za Tanzania kufuta hukumu hiyo, kumwachilia Lissu mara moja bila masharti na kukomesha matumizi ya sheria za uhaini na nyinginezo kunyamazisha wakosoaji wa serikali.

Lissu alikamatwa Aprili 9, 2025, baada ya kuhutubia mkutano wa kisiasa mjini Mbinga, kusini-magharibi mwa Tanzania.

Baadaye alishtakiwa kwa kosa la uhaini kuhusiana na machapisho yake kwenye mitandao ya kijamii yaliyowataka Watanzania kususia uchaguzi wa Oktoba 2025 kutokana na hofu ya uwezekano wa udanganyifu wa uchaguzi.

Aliachiliwa huru katika shtaka la uhaini lakini akapatikana na hatia ya uchochezi.

Share This Article