Uingereza yawatahadharisha raia wake dhidi ya kuzuru Moyale

Uingereza pia imetoa tahadhari dhidi ya safari za kwenda maeneo kadhaa ya kaskazini na mashariki mwa Kenya kutokana na vitisho vya ugaidi.

Tom Mathinji
1 Min Read
Wakimbizi kutoka Ethiopia wapokea misaada ya kibinadamu nchini Kenya.

Huku mapigano yakiendelea kushuhudiwa katika mji wa Moyale ulio kwenye mpaka wa Kenya na Ethiopia, Uingereza imetoa tahadhari dhidi ya raia wake kuzuru eneo hilo.

Kupitia Afisi ya Mambo ya Nje, jumuiya ya Madola na Maendeleo ya Uingereza (FCDO), Uingereza imesema hatua hiyo imetokana na kuzorota kwa hali ya usalama ambayo imesabishwa na mapigano kati ya pande mbili mjini Moyale eneo la Ethiopia.

“FCDO inatoa ushauri dhidi ya usafiri isipokuwa safari  muhimu katika mji wa Moyale na hadi kilomita tano kuunzunguka, pamoja na mpaka na Ethiopia,” ilisema serikali ya uingereza.

Aidha, Uingereza pia imetoa tahadhari dhidi ya safari za kwenda maeneo kadhaa ya kaskazini na mashariki mwa Kenya kutokana na vitisho vya ugaidi, hasa vinavyohusishwa na kundi la Al-Shabaab la Somalia.

Kulingana na Shirika la Msalaba Mwekundu nchini Kenya, takriban watu 36,000 wametoroka eneo la Moyale na kutafuta hifadhi upande wa Kenya, ambako wanapokea misaada ya kibinadamu.

Asasi za usalama nchini Kenya zimeongeza operesheni za kuimarisha usalama mpakani kufuatia mapigano yaliyozuka Oktoba 22 nchini Ethiopia.

Mapigano hayo yameathiri shughuli za biashara ya mpakani, uchukuzi wa bidhaa na binadamu upatikanaji wa nguvu za umeme katika mji wa Moyale, ambao inategemea kwa kiasi kikubwa umeme kutoka Ethiopia.

Share This Article