Polisi zaidi wamepelekwa kushika doria mjini Moyale, kaunti ya Marsabit katika mpaka wa Kenya na Ethiopia huku vita vikiendelea nchini Ethiopia.
Inspekta Mkuu wa Polisi Douglas Kanja ameagiza kupelekwa kwa maafisa zaidi wa polisi eneo hilo.
Kanja alitangaza kuwatuma polisi zaidi mjini Moyale baada ya kufanya mkutano wa kiusalama mjini humo siku ya Alhamisi.
Amewahakikishia wakazi wa mji huo usalama wa kutosha na kuondoa hofu ya kuzagaa kwa vita vya Ethiopia hadi Kenya.
Aidha, amewaomba raia kushirikiana na polisi na kwa kutoa taarifa za kijasusi ambazo zitasaidia kuimarisha usalama.
Kanja aliandamana na Mkurugenzi wa Idara ya Kuchunguza Kesi za Jinai Mohammed Amin, Kamanda wa GSU Johanna Tonui, na Mkurugenzi wa Operesheni za Huduma ya Kitaifa ya Polisi Philip Opiyo, miongoni mwa viongozi wengine wa kiusalama.
Watu zaidi ya 5,000 wametoroka makwao kufuatia vita vinavyoendelea nchini Ethiopia karibu na mpaka wa Kenya, hali iliyolazimisha vituo viwili vya mtihani wa kitaifa wa kidato cha nne, KCSE unaoendelea kuhamishwa kutoka Moyale kwa hofu za kiusalama.