Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka, IEBC imepata pigo baada ya Mahakama ya Kushughulikia Masuala ya Wafanyakazi mjini Malindi kusitisha mchakato unaoendelea wa kumsajili Afisa Mtendaji Mkuu mpya.
Hii ni kufuatia kesi iliyowasilishwa mahakamani na mlalamikaji Thomas Kennedy Balala kupinga mchakato huo.
Washtakiwa kwenye kesi hiyo ni IEBC, mwenyekiti wake Erastus Ethekon na wengine 11.
Jaji J.N Abuodha ameitaja kesi hiyo kuwa ya dharura na kutoa maagizo ya kusitisha mchakato wa IEBC kumsajili Afisa Mtendaji Mkuu mpya hadi kesi hiyo itakaposikilizwa Novemba 17 ikihusisha pande zote.
Maagizo hayo yanatolewa wakati ambapo kesi nyingine imewasilishwa katika Mahakama Kuu jijini Nairobi kupinga uteuzi huo, hususan kuhusika kwa kampuni ya KPMG Kenya katika uteuzi.
Kesi hiyo itatajwa Novemba 11.
Wadhifa wa Afisa Mtendaji Mkuu wa IEBC ulisalia wazi kufuatia kujiuzulu kwa Marjan Hussein Marjan mwezi Februari mwaka huu.