Bodi ya Dawa na Sumu nchini Kenya, PPB imeonya wananchi dhidi ya matumizi mabaya ya vidonge vya cetirizine.
Onyo hilo linafuatia madai potovu yanayosambazwa kwenye mitandao ya kijamii kwamba dawa hiyo ya mzio inaweza kusababisha ukavu au kubana kwa uke.
Katika tahadhari ya usalama wa umma iliyotolewa Novemba 4, 2026, bodi hiyo ilifafanua kuwa cetirizine ni dawa aina ya antihistamine inayotumika kupunguza dalili za mzio.
Dalili hizo ni pamoja na mzio wa pua na mizinga ya ngozi na inapaswa kumezwa kwa mdomo pekee kwa kufuata maelekezo ya mtaalamu wa afya aliyehitimu.
PPB ilisisitiza kuwa dawa hiyo haijaidhinishwa kutumika ukeni au kwa madhumuni ya kubana uke, huku ikibainisha kuwa hakuna ushahidi wa kisayansi unaothibitisha madai hayo.
Bodi hiyo ilionya kuwa kuingiza vidonge vya cetirizine ukeni kunaweza kusababisha muwasho, hisia za kuungua, maumivu na usumbufu.
Pia, matumizi ya dawa ambazo hazijatengenezwa kwa ajili ya matumizi ya ukeni yanaweza kuvuruga mazingira ya asili yanayolinda uke na kuongeza hatari ya maambukizi.
Aidha, kutumia cetirizine kupita kiwango kinachopendekezwa kunaweza kusababisha usingizi mwingi, kizunguzungu, kuchanganyikiwa, kutetemeka, mapigo ya moyo kwenda kasi na ugumu wa kukojoa.
PPB imewataka Wakenya kuepuka kuingiza dawa za kumeza ukeni, kuzidisha dozi zinazopendekezwa au kuamini taarifa za afya zisizothibitishwa zinazosambazwa mitandaoni.
Walio na wasiwasi kuhusu afya ya uke au masuala ya afya ya uzazi wamehimizwa kutafuta ushauri kutoka kwa wataalamu wa afya waliohitimu.