Shirika la Reli Nchini, limezindua huduma ya usafirishaji wa magari kutoka Mombasa hadi Jijini Nairobi, na kuelekea hadi Naivasha kupitia reli ya kisasa ya SGR.
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Nchini Philip Mainga, alisema huduma hiyo mpya, inafungua ukurasa mpya katika huduma ya kubeba magari nchini Kenya.
“Huu ni wakati mzuri sana wa kibiashara kwa shirika hili,” alisema Mainga, akidokeza kuwa shirika hilo limekuwa likifanya majaribio tangu mwaka jana.
Shehena ya kwanza ya usafirishaji magari, ilitekelezwa kwa ushirikiano na kampuni ya Autobarn East Africa.
Mkurugenzi huyo alitoa wito kwa wadau katika sekta ya magari kutumia mfumo huo mpya wa usafirishaji wa magari kutumia reli ya kisasa.
“Tunawahimiza waagizaji wa magari na mawakala, wafanyekazi nasi,” alisema Mainga.
Kulingana na Mainga, huduma hiyo ni salama, yenye gharama nafuu kwa wafanyabiashara, waagizaji magari na wasambazaji wa magari kulinganishwa kwa usafirishaji wa barabarani.