Watu 302 wahama makwao kutokana na mafuriko Tana River

Mafuriko hayo yalikumba eneo la Tana Delta baada ya mabwawa ya Tulu na Minjila kufurika, na kusomba nyumba pamoja na maeneo ya makazi.

Tom Mathinji
1 Min Read
Watu zaidi ya 300 wahama makwao kutokana na mafuriko Tana River.

Shirika la Msalaba Mwekundu limesema kuwa zaidi ya watu 300 wamehama makwao, baada ya mabwawa kufurika katika kaunti ya Tana River. 

Kulingana na shirika hilo mafuriko hayo yalikumba eneo la Tana Delta baada ya mabwawa ya Tulu na Minjila kufurika, na kusomba nyumba pamoja na maeneo ya makazi.

Kati ya familia 302 zilizolazimika kuhama, familia 175 zimepokea chakula na blanketi kupitia msaada kutoka kwa serikali ya kitaifa na ile ya kaunti.

Shirika hilo limesema familia zilizosalia zinatarajiwa kupokea msaada wa kibinadamu, huku mafuriko hayo yakiripotiwa kuenea hadi kaunti jirani ya Lamu, ambapo nyumba katika maeneo ya Hindi na Witu zimeathirika.

Aidha, shirika hilo pia limedokeza kuwa watu takriban 3,000 wameathirika kutokana na mvua inayonyesha katika eneo la pwani, likisema makundi yake bado yako nyanjani kutathmini hali hiyo na kuratibu shughuli za utoaji misaada.

Hata hivyo, limesema kuwa familia zaidi huenda zikalazimika kuhama makazi yao.

Share This Article