Rais William Ruto leo Jumamosi amezindua mikradi kadhaa ya miundombinu, kwenye siku ya kwanza ya ziara yake katika eneo la Ukambani.
Kiongozi huyo wa taifa alizindua mradi wa maji wa thamani ya shilingi bilioni 1.47 katika kaunti ya Machakos, ambao una uwezo wa kusambaza lita milioni 6.6 za maji kila siku.
Kulingana na Rais Ruto, mradi huo utawanufaisha wakazi 137,400 pamoja na taasisi 10 katika maeneo 10.
“Awamu ya pili ya mradi huo utakaogarimu shilingi milioni 500, utaongeza usambazaji wa maji kwa wakazi 120,000 zaidi katika eneo bunge la Mwala,” alisema Rais Ruto.
Akizungumza na wananchi katika eneo la Mwala baada ya uzinduzi wa mradi huo wa maji, Rais Ruto alidokeza kuwa serikali inajenga barabara 10 mpya katika kaunti ya Machakos itakayogharimu kitita cha shilingi bilioni 21.
Katika kaunti ya Makueni, kiongozi wa taifa alizindua ujenzi wa barabara ya Kyambeke-Kyuasini-Ukia utakaogharimu shilingi bilioni 1.4, pamoja na kuanzisha utumizi wa barabara ya Kyambeke-Kikoko iliyogharimu shilingi bilioni 1.5 katika eneo bunge la Kaiti.

“Tunawekeza shilingi bilioni 16 kwa ujenzi wa barabara mpya ya umbali wa kilomita 180 katika kaunti ya Makueni, ili kufungua eneo hilo, kuimarisha uunganishaji na kubuni fursa za kiuchumi,” alisema Rais Ruto.
Rais Ruto alisisitiza umuhimu wa viongozi wa ngazi za mashinani kushirikiana na serikali ya kitaifa, ili kuharakisha utekelezaji wa miradi ya maendeleo na utoaji wa huduma kwa wananchi.
Kiongozi huyo wa taifa yuko kwenye ziara ya maendeleo ya siku nne katika eneo la Ukambani.