MCA akamatwa kwa madai ya kuhusika kwa wizi wa simu Nairobi

Cyrus Kisavi Musyoka, alikamatwa na Maafisa wa Polisi kutoka kituo cha Kamukunji baada ya kuhusishwa na visa kadhaa vilivyoripotiwa vya wizi wa simu.

Tom Mathinji
1 Min Read
Mwajilishi wadi ya Ikanga/Kyatune kaunti ya Kitui, Cyrus Kisavi Musyoka, akamatwa kwa madai ya wizi wa simu.

Mwakilishi wadi ya Ikanga/Kyatune iliyo katika kaunti ya Kitui, amekamatwa Jijini Nairobi kwa madai ya kuhusika katika msururu wa wizi wa simu.

Cyrus Kisavi Musyoka, alikamatwa na Maafisa wa Polisi kutoka kituo cha Kamukunji baada ya kuhusishwa na visa kadhaa vilivyoripotiwa vya wizi wa simu.

Idara ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), kwenye ukurasa wake wa X, imesema mshukiwa huyo amekuwa akichunguzwa kufuatia visa tofauti vya wizi wa simu vilivyotekelezwa kati  ya mwezi Agosti na Septemba mwaka 2026.

“Kamera fiche za CCTV zilifanikisha pakubwa uchunguzi wetu, huku maafisa wakimtambua na kumhusisha na matukio hayo,” ilisema DCI.

Kulingana na DCI, mshukiwa huyo pia anakabiliwa na agizo la kufika mahakamani kwenye kesi tofauti ya wizi inayomkabili.

“MCA anakabiliwa na agizo la kufika mahakamani kwenye kesi ya uhalifu nambari 112/303/2024,  baada ya kukosa kufika katika mahakama ya Makadara baada ya kuachiliwa kwa dhamana,” iliongeza DCI.

Mshukiwa huyo anazuiliwa kwenye korokoro za polisi, akisubiri kufikishwa mahakamani.

Share This Article