Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC), imepata maagizo ya kutwaa mali ya thamani ya shilingi milioni 207,741,928, inayomilikiwa na mfanyakazi wa zamani wa serikali ya kaunti ya Trans Nzoia.
Kwenye maagizo yaliyotolewa tarehe nane Oktoba na Jaji Rose Ougo wa mahakama ya kushughulikia ufisadi na uhalifu wa kiuchumi, Andrew Biketi Musuya alishindwa kufafanua kikamilifu umiliki wa mali hiyo ikilinganishwa na mshahara wake unaojulikana.
Mali hiyo inajumuisha majengo mawili katika kaunti za Mombasa na Bungoma yenye thamani ya shilingi 150, 209,000, majengo mawili ya gorofa tano eneo la Mtwapa, nyumba yenye vyumba vitano vya malazi katika eneo hilo na vipande saba vya ardhi Mombasa na Bungoma.
Maafisa wa uchunguzi wa EACC, walibaini kuwa, kati ya mwezi January mwaka 2013 na Oktoba 2018, Musuya alipata mali hiyo yenye jumla ya thamani ya 289,932,910.
“Hii inajumuisha fedha kwenye akaunti ya benki na Mpesa ambazo ni shilingi 53,532,910, ardhi ya thamani ya shilingi 226.8 na magari ya thamani ya shilingi milioni 9.6 millio,” ilisema EACC.
Mahakama ilisema mali hiyo yote itwaliwe na serikali.