Kenya imeimarisha ulinzi wa watoto mitandaoni, asema Ruto

Rais alisema ulinzi wa watoto mtandaoni umeimarishwa kupitia mazungumzo ya kitaifa yanayowajumuisha watoto, familia, wasomi, kampuni za teknolojia na serikali.

Tom Mathinji
1 Min Read
William Ruto- Rais wa Kenya.

Rais William Ruto amesema Kenya imeimarisha ulinzi wa watoto mitandaoni kupitia sheria, sera na mikakati mwafaka ya Akili Unde (AI), huku ikihakikisha watoto wanafaidika kikamilifu kutokana na teknolojia.

Kiongozi huyo wa taifa alisema ulinzi huo wa watoto mtandaoni pia umeimarishwa kupitia mazungumzo ya kitaifa yanayowajumuisha watoto, familia, wasomi, kampuni za teknolojia na serikali.

Akizungumza kwenye mkutano wa viongozi wa ngazi za juu katika Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa Jijini New York,  Rais Ruto alisema Kenya ikiwa mwanzilishi mwanachama wa Muungano wa Ulinzi wa Haki za Watoto katika enzi ya Akili Unde, usalama wa kiteknolojia unapaswa kubuniwa kuanzia mwanzo.

“Hakuna mtoto anapaswa kuchagua kati ya kuunganishwa kwenye mtandao na kuwa salama. Huku Akili Unde inavyobadilisha masomo ya watoto, usalama unapaswa kuzingatiwa kuanzia mwanzo,” alisema Rais Ruto.

Rais Ruto yuko nchini Marekani, ambako amejiunga na viongozi wengine wa dunia, kuhudhuria mkutano wa 81 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa (UNGA).

Share This Article