Rais wa Sudan Kusini, Salva Kiir, ameivunja serikali ya mpito ya nchi hiyo miezi mitatu kabla ya uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Desemba 22.
Hatua hiyo inamaanisha kuwa muda wa serikali ya mpito unamalizika rasmi saa sita usiku wa leo Jumanne, kufuatia kuanza kutumika kwa marekebisho ya Sheria ya Uchaguzi ya Kitaifa yaliyopitishwa na kutiwa saini na Kiir.
Sheria hiyo inamruhusu rais aliyepo madarakani kuendelea kutekeleza majukumu yake kwa mamlaka kamili ya kikatiba katika kipindi cha uchaguzi hadi rais mpya atakapochaguliwa na kuapishwa. Pia inampa mamlaka ya kuwaondoa madarakani makamu wote watano wa rais, akiwemo Makamu wa Kwanza wa Rais Riek Machar, ndani ya miezi mitatu kabla ya uchaguzi.
Aidha, sheria hiyo inaelekeza kuvunjwa kwa Bunge la Kitaifa, mabunge ya majimbo na serikali za kitaifa na za majimbo.
Serikali imesema hatua hiyo ni sehemu ya maandalizi ya uchaguzi na imesisitiza kuwa makubaliano ya amani ya mwaka 2018 bado yanaendelea kutekelezwa.
Uchaguzi wa Desemba 22 unatarajiwa kuwa wa kwanza wa kitaifa tangu Sudan Kusini ipate uhuru mwaka 2011, baada ya kuahirishwa mara kadhaa tangu kutiwa saini kwa makubaliano ya amani mwaka 2018.
Taarifa ya BBC