Serikali inapanga kuchukua hatua kadhaa zinazolenga kuokoa Ziwa Baringo, kulingana na Katibu wa Ulinzi Patrick Mariru.
Katibu Mariru, alitangaza mpango huo jana Jumanne wakati wa ziara ya ukaguzi katika Maziwa Baringo na Bogoria, ambapo alikuwa ameandamana na mwenzake wa Umwagiliaji Ephantus Kimotho.
Tatizo katika ziwa Baringo ni kuendelea kuongezeka kwa kina cha maji ambapo sasa serikali inadhamiria kujenga handaki na mfereji.
Hiyo ni ishara ya mabadiliko kutoka kwa hatua za kukabiliana na majanga hadi suluhisho za muda mrefu za miundombinu zinazolenga kulinda jamii, kuhifadhi mazingira na kufungua fursa za kilimo katika eneo hilo.
Ziara hiyo ilikuwa sehemu ya tathmini ya awali ya kuthibitisha kiwango cha mafuriko na kukamilisha mipango ya uhandisi kabla ya kuanza kwa ujenzi.
Mariru alisema kuwa hatua hiyo inalenga kupunguza mafuriko, kuhifadhi bioanuwai, kulinda maisha na riziki za wananchi na kuunda fursa za maendeleo ya kiuchumi kupitia miradi ya umwagiliaji.
Tangu mwaka 2010 kiwango cha maji kimezidi kuongezeka katika Ziwa Baringo hali iliyosababisha nyumba, shule, barabara, mashamba, vituo vya utalii na miundombinu mingine ya umma kufunikwa na maji.
Mafuriko hayo yamewalazimu maelfu ya wakazi kuhama na kuvuruga shughuli zao za kujipatia riziki.
Serikali pia imeonya kuhusu hatari inayoongezeka ya Maziwa Baringo na Bogoria kuungana iwapo hatua za haraka hazitachukuliwa.
Maafisa walisema kuwa tukio hilo lingeunganisha mfumo wa maji safi wa Ziwa Baringo na maji yenye chumvi na alkali ya Ziwa Bogoria, jambo ambalo lingeleta athari kubwa kwa mazingira kwa kuharibu bioanuwai, kupunguza utalii na kudhoofisha shughuli za kiuchumi katika eneo hilo.