Kenya imeashiria utayari wake wa kuongeza biashara ya mahindi na Uganda wakati nchi hizo mbili zikilenga kuzidisha biashara ya kilimo chini ya makubaliano yanayodhamiria kuunda eneo la biashara huru miongoni mwa nchi za bara la Afrika, AfCFTA.
Utayari huo umeelezewa wakati ambapo kumekuwa na hofu ya Kenya kukumbwa na uhaba wa mahindi kutokana na uzalishaji mbovu wa zao hilo uliosababishwa na ukame katika maeneo mbalimbali nchini msimu wa upanzi uliopita.
Waziri wa Kilimo Mutahi Kagwe amesema Uganda iko katika nafasi nzuri ya kukidhi sehemu ya mahitaji ya Kenya ya mahindi.
Hata hivyo, ameitaka nchi hiyo kuimarisha mbinu za kuwasaidia wakulima kukausha mahindi ipasavyo na kuangazia wasiwasi wa bidhaa hiyo kuwa na sumu ya aflatoxin kabla ya kuingizwa humu nchini.
Kagwe aliyasema hayo wakati wa hafla ya chakula cha mchana iliyoandaliwa Kamati ya Kilimo ya Bunge la Uganda katika hoteli moja jijini Nairobi jana Jumatatu.
Kulingana naye, kuboresha ushughulikiaji wa mazao baada ya mavuno utafaidi nchi hizo mbili kwa kufungua fursa kubwa kwenye soko kwa wakulima wa Uganda wakati ukihakikisha walaji nchini Kenya wanapokea chakula salama na cha ubora wa hali ya juu.
“Tunahitaji mfumo nchini Uganda ambapo mahindi yanakaushwa kabla ya kuvuka mpaka,” alishauri Kagwe.
“Tunaweza kununua, lakini tunahitaji mahindi yasiyokuwa na sumu ya aflatoxin.”
Kwa upande wake, ujumbe wa Uganda ulitoa wito wa kuwianishwa kwa taratibu za kilimo na biashara, ikiwa ni pamoja na ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, ili kuwezesha usafirishaji wa mazao wakati pia viwango vya usalama na ubora vikudumishwa.
Ujumbe huo ulitaja mabadiliko ya tabia nchi, maji ya uzalishaji, udhibiti wa wadudu na magonjwa, uhifadhi kwenye vipozea, huduma za nyanjani, masoko hafifu na uongezeaji thamani kuwa miongoni mwa changamoto zinazohitaji uwekezaji mkubwa na ushirikiano wa kikanda.