Gavana Kachapin alaani vurugu za Sigor

Kiongozi huyo anazitaka idara za usalama kuchunguza tukio hilo na kuwakamata waliohusika

Marion Bosire
1 Min Read

Gavana wa kaunti ya Pokot Magharibi, Simon Kachapin, amelaani ghasia zilizovuruga ziara ya Rais William Ruto ya kuzuru miradi ya maendeleo katika eneo la Sigor wiki iliyopita.

Kiongozi huyo anazitaka idara za usalama kuchunguza tukio hilo na kuwakamata waliohusika.

Akizungumza wakati wa sherehe za Siku Kuu ya Mashujaa, Kachapin alisema waliohusika katika makabiliano kati ya makundi hasimu ya kisiasa, yaliyosababisha kifo cha mtu mmoja, wanapaswa kukamatwa na kufikishwa mahakamani.

Alisema kuwawajibisha wahusika kutasaidia kuzuia ghasia za kisiasa na kuzuia vifo zaidi.

Gavana huyo alionya kuwa tukio hilo linaweza kuweka mfano hatari wa kuvuruga shughuli za Rais, akisisitiza kuwa tofauti za kisiasa hazipaswi kugeuka kuwa vurugu.

“Maisha ya mtu mmoja yamekatizwa, na wanafamilia wanaomboleza kwa sababu ya siasa,” alisema Kachapin.

Aliwataka wanasiasa kuwasilisha ajenda zao kwa wapiga kura kwa njia ya amani, akiongeza kuwa hakuna haja ya kutumia vurugu ili kiongozi yeyote apate umaarufu au aonekane kama shujaa.

Kachapin aliwahimiza viongozi wa kisiasa kukumbatia uvumilivu na kampeni zinazojikita katika masuala muhimu kwa wananchi badala ya kuchochea wafuasi wao dhidi ya wapinzani.

Share This Article