Serikali ya Tanzania imeimarisha masharti ya afya kwa wasafiri wanaoingia nchini humo, kufuatia mlipuko wa Ebola katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, DRC na visa kadhaa nchini Kenya.
Katika mwongozo uliotolewa Oktoba 17, 2026, Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya ya Tanzania, Dkt. Grace E. Magembe, alisema wasafiri wote wanapaswa kujaza Fomu ya Ufuatiliaji wa Afya ya Msafiri mtandaoni kabla ya kuanza safari au wanapowasili nchini humo.
Wasafiri pia watafanyiwa uchunguzi wa afya, ikiwemo kupimwa joto la mwili katika viwanja vya ndege, mipaka ya nchi kavu na bandari za taifa hilo la Afrika Mashariki.
Aidha, wasafiri walio katika hatari kubwa watafuatiliwa kwa siku 21, huku wakitakiwa kushirikiana na mamlaka za afya na kujibu jumbe za ufuatiliaji hata baada ya kuondoka nchini Tanzania.
Serikali hiyo, imewataka wasafiri kuripoti dalili za ugonjwa wa Ebola au magonjwa mengine ya kuambukizwa katika vituo vya afya vilivyo karibu au kupiga simu kwa nambari 199 ambayo ni ya bila malipo.
Wasafiri na waendeshaji wa vyombo vya usafiri pia wametakiwa kuzingatia usafi wa mikono, kutumia vitakasa mikono na kuepuka misongamano isiyo ya lazima.
Kwa mujibu wa mwongozo huo, hatua hizo zimeanza kutekelezwa mara moja na zitapitiwa mara kwa mara kulingana na hali ya mlipuko.