Kisa cha kushangaza kimetokea huko mkoani Arusha nchini Tanzania baada ya mama fulani kuhama nyumba aliyopangisha kwa takribani miaka 17!
Kulingana na wanahabari wa nchi hiyo, baadhi ya wakazi wa mtaa wa Elkiroa, kata ya Lemara mkoani Arusha, wameandaa sherehe kubwa kufurahikia hatua ya mwenzao kuhama.
Walipika vyakula vingi kusherehekea kuondoka kwa Mama Rashid wiki kadhaa baada ya kumtuhumu kuhusika na vitendo vya ushirikina na kung’ang’ania nyumba zinazodaiwa kuwa mali ya marehemu.
Alipohojiwa na wanahabari awali, Mama Rashid alidai kwamba alikataa kuondoka kwa sababu alikuwa akimdai msimamizi wa mali ya mwendazake anayeaminika kuwa mmiliki wa nyumba hiyo, kiasi cha shilingi milioni saba.
Yapata wiki moja iliyopita, Mama huyo alihojiwa na wanahabari baada ya kuvunjiwa nyumba husika ambapo alisema kwamba alimkopesha mmiliki wa nyumba hiyo pesa hizo alipokuwa akiuguza mtoto.
“Nilienda kikoba nikachukua milioni saba nikampa mama mwenye nyumba, wakati huo alikuwa anamuuguza Mtoto wake kwa miaka mitatu hadi akafariki,” amesema Mama Rashid.
Polisi wa Kata ya Lemara hata hivyo waliingilia kati na kuonya wakazi dhidi ya kujichukulia sheria mkononi na badala yake kufuata taratibu za kisheria.
Majirani waliohojiwa walimtaja kuwa mchawi na mchonganishi.