Chama tawala nchini Tanzania CCM kimefanya mabadiliko madogo katika uongozi wake, kufuatia kikao kilichoandaliwa jana Oktoba 11, 2026 huko Kizimkazi, Zanzibar.
Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Chama cha Mapinduzi, CCM, Taifa ilifanya uteuzi wa Viongozi mbalimbali pamoja na mabadiliko ya Walezi wa Mikoa kwenye kikao hicho.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa, NEC, Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Kenani Laban Kihongosi, Kamati Kuu ilimteua Dkt. Nettho Ndijina Ndilito kuwa Mgombea wa Ubunge kupitia CCM katika Uchaguzi Mdogo wa Jimbo la Chamwino, Mkoa wa Dodoma.
Uchaguzi huo wa Novemba 4, 2026, umesababishwa na hatua ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kumteua aliyekuwa mbunge wa Chamwino, Deogratius John Ndejembi, kuwa Makamu wa Rais Agosti 28, 2026.
Katika uteuzi mwingine, Kamati Kuu imemteua Faris Buruhani kuwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi, UVCCM, ambapo kabla ya uteuzi huo, Faris alikuwa Mwenyekiti wa UVCCM Mkoa wa Kagera.
Aidha, Kamati Kuu imefanya mabadiliko madogo ya Walezi wa Mikoa, ambapo Deogratius John Ndejembi ameteuliwa kuwa Mlezi wa CCM Mkoa wa Dar es salaam, huku Kenani Laban Kihongosi akiteuliwa kuwa Mlezi wa CCM Mkoa wa Dodoma.