Maafisa wa Polisi wamemkamata mshukiwa wa ulanguzi wa mihadarati katika kaunti ya Busia.
Baada ya kupokea habari za kijasusi, maafisa hao walimkamata Titus Okware mwenye umri wa miaka 25, alipokuwa akiabiri basi ili kusafirisha mihadarati hiyo hadi Jijini Nairobi.
Mkoba wake mdogo haukuashiria hatari yoyote hadi pale polisi walipoupekua na kupata bangi iliyokuwa imefichwa kwenye boksi za kuweka simu za mkononi, licha ya kuwa hakukuwa na simu ndani.
Maafisa hao walipata vipande 1,121 vya bangi, huku mshukiwa huyo akizuiliwa katika kituo cha polisi cha Busia akisubiri kuwasilishwa mahakamani.
Mihadarati hiyo inazuiliwa kama ushahidi utakaotumiwa kwenye kesi dhidi ya mshukiwa huyo.