Marioo arejea Tanzania kwa kishindo baada ya ushindi wa AFRIMMA

Alilakiwa na watu wengi wenye uwanja wa ndege wa kimataifa wa Julius Nyerere wakiwemo wanahabari na mpenzi wake Paula.

Marion Bosire
1 Min Read

Msanii nyota wa Bongo Flava, Marioo, amerejea nchini Tanzania kutoka Marekani ambapo amekuwa tangu alipokwenda kwa ajili ya tuzo za AFRIMMA.

Marioo alilakiwa na watu wengi wenye uwanja wa ndege wakiwemo wanahabari, mpenzi wake Paula na mama mkwe Fridah Kajala, baada ya kufanya vizuri kwenye ziara yake ya kimuziki na kufanikiwa kutwaa tuzo kubwa ya kimataifa ya AFRIMMA.

Msanii huyo alitwaa tuzo ya Msanii Bora wa Kiume Afrika Mashariki yaani Best Male Artist in East Africa katika kilele cha utoaji wa tuzo hizo jijini Dallas, Texas, Septemba 12, 2026.

Katika kipengele hicho, Marioo aliwashinda wasanii wakubwa wa ukanda huu, kama Diamond Platnumz na Jux wa Tanzania na Bien wa Kenya.

Akizungumza na waandishi wa habari katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Marioo alimshukuru Mungu na mashabiki wake kwa kumpigia kura.

Nyota huyo alibainisha kuwa ziara hiyo ya mwezi mmoja imefungua milango mikubwa kwenye safari yake ya muziki kimataifa kwani ilikuwa ziara yake ya kwanza nchini Marekani.

Kurejea kwake kumeleta faraja kubwa kwa sekta ya sanaa nchini Tanzania huku akipongezwa kwa kuipeperusha vyema bendera ya Taifa hilo la Afrika Mashariki. .

Share This Article