Utekelezaji wa sheria za trafiki waimarishwa

Hatua hii inafuatia ongezeko la ajali za barabarani nchini.

Marion Bosire
2 Min Read
Inspekta Jenerali wa Polisi Douglas kanja.

Huduma ya Taifa ya Polisi, NPS imeimarisha uhamasishaji na utekelezaji wa sheria za usalama barabarani kufuatia ongezeko la ajali za barabarani nchini.

Katika taarifa iliyotolewa Oktoba 6, 2026, msemaji wa NPS Muchiri Nyaga alisema ajali hizo zimesababisha vifo, majeraha mabaya, uharibifu wa mali na madhara mengine makubwa.

Kulingana na Polisi ajali nyingi zinasababishwa na makosa ya kibinadamu, yakiwemo kuendesha kwa uzembe na kupita magari bila tahadhari, mwendo kasi, uchovu wa madereva na kuendesha gari wakiwa wamelewa au kutumia dawa za kulevya.

Nyaga aliwataka madereva, waendesha pikipiki, waendesha baiskeli na wanaotembea kwa miguu kuwa waangalifu na kuzingatia kikamilifu sheria za barabarani.

Pia aliwaagiza maafisa wa trafiki kuwa macho, kudhihirisha weledi na kuchukua hatua katika kutekeleza sheria za usalama barabarani na kulinda wanaotumia barabara.

NPS ilisema itashirikiana na wadau wengine wa sekta ya usafiri kuimarisha utekelezaji wa sheria na kampeni za uhamasishaji wa umma, pamoja na operesheni maalum kote nchini.

Huduma hiyo imewataka wananchi kuripoti tabia za kutiliwa shaka au uendeshaji hatari katika kituo cha polisi kilicho karibu au kupitia nambari za dharura 999 na 911.

Ripoti za siri zinaweza pia kutolewa kupitia #FichuaKwaDCI kwa 0800 722 203 au WhatsApp 0709 570 000.

NPS imesema usalama barabarani ni jukumu la kila mtu na kuwataka watumiaji wote wa barabara kuchukua hatua kulinda maisha.

Share This Article