Kenya na Rwanda zilitoka sare kappa katika mchuano wa kimataifa wa kirafiki uliopigwa Jumatatu jioni katika uwanja wa Amahoro,mjini Kigali.
Amavubi Stars na Harambee Stars walibuni nafasi haba za kupachika magoli katika dakika 90 za mchuano huo.
Rwanda wanaokalia nafasi ya 128 ulimwenguni waliingia mechi hiyo roho juu baada ya kuzoa pointi sita kutoka na mechi mbili za kundi K kufuzu Kombe la AFCON mwaka ujao.
Rwanda waliishinda Liberia mabao 3-1 katika mechi ya kwanza ,kabla ya kuwalemea Cape Verde 2-1 ugenini katika mchuano wa pili.
Kenya upande wake licha ya kuwa tayari imefuzu kama mwenyeji wa fainali hizo wanaburura mkia kundini D, kwa pointi moja baada ya kutoka sare nyumbani na Eritrea, kabla ya kuambulia kichapo cha moja nunge ugenini kwa Guinea.
Harambee stars yake Benni McCarthy ni ya 109 katika msimamo wa FIFA duniani.
Rwanda watazuru Mali kwa mechi ya tatu Novemba 11 timu zote zikiongoza kundi hilo kwa alama sita wakati Kenya wakiwa ugenini dhidi ya Afrika Kusini siku iyo hiyo.