Rais William Ruto ameagiza kwamba maafisa wote wa umma wanaostaafu walipwe pensheni ndani ya siku 10 baada ya kustaafu.
Maafisa hao wamekuwa wakihangaika kwa miaka na mikaka wakidai malipo yao ya pensheni kiasi cha baadhi yao kufariki bila kuonja utamu wa kile walichokifanyia kazi kwa miaka mingi.
“Nimetoa maagizo bayana kwa Hazina ya Taifa ya Malipo ya Uzeeni, NSSF kwamba kuanzia sasa, malipo yote ya kustaafu ya wafanyakazi wote wa umma lazima yawe tayari na kulipwa ndani ya siku 10 baada ya kustaafu,” alisema Rais Ruto alipowahutubia walimu leo Jumatatu.
Akizungumza wakati wa maadhimisho ya Siku ya Walimu Duniani yaliyoandaliwa katika uwanja wa Kasarani, Ruto alisema kinyume cha awali, utawala wake umeweka mikakati ya kuhakikisha hakuna mwalimu wala afisa wa umma atakayehangaika akitafuta malipo yake baada ya kustaafu.
“Tumesema, mwalimu kama anaenda retire, asihangaike barabarani kutoka ofisi moja ama nyingine, asihangaike akitafuta sijui mbunge ama nani,” alisema Rais Ruto wakati akishangiliwa na hadhira.
Huku akisisitiza kuwa wastaafu wanapaswa kuishi maisha ya heshima baada ya kutumikia taifa, Rais alidokeza kuwa Julai 1 mwaka huu, Tume ya Kuwaajiri Walimu, TSC na Wizara ya Fedha zilizindua Mfumo wa Usimamizi wa Pensheni utakaosaidia kuharakisha utoaji malipo ya pensheni huku rekodi za wastaafu kwa sasa zikiwekwa kwenye mfumo huo.
Taasisi zinazohusika na utayarishaji wa mfumo huo zinasema utakuwa tayari kutumika kikamilifu ndani ya miezi mitatu.
Mfumo huo unalenga kuhakikisha walimu wanaostaafu wanapokea malipo yao ya kustaafu ndani ya siku 10 baada ya kustaafu.