Kenya imepiga hatua muhimu katika kuimarisha uhusiano wake na Saudi Arabia baada ya Mkuu wa Mawaziri na Waziri wa Mambo ya Nje, Musalia Mudavadi, kuwasili jijini Riyadh.
Mudavadi yuko nchini humo kwa ajili ya Mashauriano ya Kwanza ya Kisiasa kati ya mataifa hayo mawili.
Mazungumzo hayo ya ngazi ya juu, yanayoongozwa na Waziri wa Mambo ya Nje wa Saudi Arabia, Mwanamfalme Faisal bin Farhan Al Saud, yanatarajiwa kuweka msingi wa ushirikiano wa karibu zaidi katika biashara, uwekezaji, uhamaji wa wafanyakazi, amani na usalama huku mataifa hayo yakilenga kuimarisha ushirikiano wao wa kimkakati.
Mudavadi anaongoza ujumbe wa Kenya unaojumuisha Waziri wa Leba na Ulinzi wa Jamii Alfred Mutua, Makatibu wa wizara Profesa Shaukat Abdulrazak na Roseline Kathure Njogu, Balozi wa Kenya nchini Saudi Arabia Joseph Masila pamoja na Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Mashariki ya Kati katika Wizara ya Mambo ya Nje, Lindsay Kiptiness.
Mazungumzo hayo yanatarajiwa kuhitimishwa kwa Tamko la Pamoja na kutiwa saini kwa Hati kadhaa za Makubaliano zitakazoongeza ushirikiano katika sekta mbalimbali na kufungua fursa mpya za maendeleo kwa mataifa yote mawili.
Mbali na mashauriano hayo, Mudavadi anatarajiwa kukutana na viongozi wa kampuni ya Saudi Aramco, kufanya mazungumzo na Wakenya wanaoishi nchini Saudi Arabia, na kuhutubia Kongamano la Biashara kati ya Kenya na Saudi Arabia.
Kongamano hilo liliandaliwa kwa ushirikiano na Shirikisho la Vyama vya Wafanyabiashara la Saudi Arabia na Chama cha Kitaifa cha Wafanyabiashara na Viwanda cha Kenya.
Ziara hiyo inaonyesha juhudi za Kenya za kuimarisha ushirikiano wake na mataifa ya Ghuba kwa lengo la kuvutia uwekezaji, kupanua fursa za ajira kwa wananchi wake, kuongeza mauzo ya bidhaa nje ya nchi na kuimarisha ushirikiano wa kimataifa unaochochea ajenda ya ukuaji endelevu wa uchumi wa muda mrefu.