Waandaaji wa tamasha maarufu ya Kenya ya KULTURE, wametangaza kuahirishwa kwa awamu ya tatu ya tamasha hiyo iliyokuwa imepangwa kuandaliwa Oktoba 10, 2026.
Bila kutoa tarehe mbadala, waandaaji hao wameahirisha tamasha hiyo iliyostahili kufanyika katika jumba la Mikutano ya Kimataifa la Kenyatta, KICC.
Katika taarifa rasmi, waandaaji walielezea kwamba walifahamishwa na usimamizi wa KICC kwamba eneo hilo litakuwa mwenyeji wa tukio la serikali katika siku chache kabla ya tamasha hiyo.
Hali hiyo inatarajiwa kupunguza kwa kiasi kikubwa muda wa maandalizi ya ukumbi, uzalishaji wa kiufundi, majaribio ya sauti na mazoezi kwa ajili ya tamasha ya KULTURE 3.
Waandaaji walisema muda huo mfupi uliobaki wa maandalizi ungefanya iwe vigumu kuandaa tamasha hilo kwa kiwango walichoahidi watazamaji.
“Afadhali tuahirishe kuliko kuathiri ubora wa tamasha,” waandaaji hao walisema.
Wote waliokuwa wamenunua tiketi kwa ajili ya KULTURE 3 watarejeshewa fedha kamili ndani ya siku saba na maelezo zaidi yatatolewa moja kwa moja kwa walio na tiketi.
Waandaaji waliwashukuru mashabiki, wasanii, washirika, washirikishi na wote waliohusika katika maandalizi ya tukio hilo, huku wakiomba radhi kwa kuahirishwa kwake.
Kundi hilo limesema linatarajia kufanikisha tamasha hiyo kama ilivyokusudiwa awali pindi mazingira yatakaporuhusu.