Mwanamitindo wa asili ya Uganda Zari Hassan amekanusha madai kwamba alimfurusha mwanamuziki mashuhuri wa taifa hilo Jose Chameleone kutoa kwenye sherehe yake ya siku ya kuzaliwa.
Mrembo huyo alikuwa anaadhimisha mwanzo wa mwaka wake wa 46 maishani alipoonekana kwenye video zilizonakiliwa katika eneo la tukio akielekeza walinzi kufurusha watu fulani.
Baadaye ilibainika kwamba watu hao walikuwa na mavazi ambayo kulingana naye hayakukidhi hadhi ya kuwa kwenye sherehe hiyo huku wanamitandao wakidai kwamba Jose Chameleone ni miongoni mwa waliofurushwa.
Zari hata hivyo amekanusha madai hayo akisisitiza kwamba watu ambao alitaka waondolewe walikuwa watatu na mwonekano wao haukuafikia kiwango alichokuwa ameweka, na Jose hakuwa mmoja wao.
“Haikuwa Chameleone. Ilikuwa watu watatu nisiowafahamu waliokuwa wamejivaa kiholela holela,” alisema Zari.
Kulingana naye wageni husika walikuwa wamevaa mashati tao yasiyo na mvuto na viatu vichafu, hali iliyomkera na kusababisha aelekeze walinzi wawaondoe.
Zari alisisitiza kwamba ana urafiki wa muda mrefu na Chameleone na kamwe hawezi kumdhulumu namna hiyo katika sherehe ya siku yake ya kuzaliwa.
Analaumu wanaoeneza uvumi huo mitandaoni akisema kwamba wanajitafutia umaarufu tu na suala hilo, huku maneno yao yakikwaza urafiki wa miaka mingi.
Mrembo huyo ameahidi pia kutafuta video inayoonyesha watu halisi alioelekeza waondolewe na kuichapisha ili kutatua suala hili kabisa.