Madereva wakubali kusitisha mgomo Tanzania

Hatua hii inafuatia kikao kilichoandaliwa na Waziri Mkuu wa Tanzania Dkt. Mwigulu Nchemba na viongozi wa madereva hao wa mabasi na malori.

Marion Bosire
1 Min Read
Mwigulu Nchemba, Waziri Mkuu wa Tanzania

Taarifa za hivi punde kutoka Tanzania zinaashiria kwamba madereva wa mabasi na malori nchini humo wamekubali kusitisha mgomo wao uliodumu siku mbili.

Hatua hii inafuatia kikao kilichoandaliwa na Waziri Mkuu wa Tanzania Dkt. Mwigulu Nchemba na viongozi wa madereva hao ambapo walikubali kurejesha huduma za usafiri.

Mazungumzo hayo yamefanyika leo Septemba 30, 2026, katika Ofisi Ndogo ya Waziri Mkuu, katika eneo la Oysterbay jijini Dar es Salaam.

Serikali ya Tanzania iko tayari sasa kusikiliza na kufanyia kazi changamoto zinazowakabili madereva, huku majadiliano yakiendelea kati ya Serikali na wadau husika.

Madereva hao waliamua kususia kazi kutokana na hatua ya maafisa wa polisi wanaohusika na usalama barabarani kuwakata au kuwapunguzia alama kwenye leseni zao kila wanapofanya kosa barabarani.

Walilalamikia pia suala la faini za barabarani na changamoto nyingine zinazohusiana na usimamizi wa sheria za usalama barabarani.

Mgomo huu ulioanza jana Septemba 29, 2026, ulisababisha abiria kukwama katika vituo mbalimbali vya mabasi nchini Tanzania na kuathiri shughuli za usafirishaji wa mizigo na biashara.

Jana jioni Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi ya Tanzania, Patrobas Katambi aliagiza kusitishwa kwa mfumo huo wa alama au pointi kwa Madereva, akifafanua kwamba ulikuwa haujaanza kutekelezwa rasmi bali ulikuwa katika hatua ya majaribio.

Share This Article