Bodi ya Hakimiliki ya Kenya, KECOBO, imetangaza kuahirishwa kwa kikao cha kushirikisha umma kilichokuwa kimetangazwa awali kutathmini mashirika yanayoomba leseni.
Katika taarifa kwenye mitandao ya kijamii leo, KECOBO ilisema kwamba hatua hii imechochewa na agizo la mahakama kuu ya Kiambu lililotokana na kesi nambari E109 ya mwaka 2026.
“Kufuatia agizo la mahakama lililotolewa na Mahakama Kuu ya Kiambu (Ombi nambari. E109 la 2026), bodi ingependa kufahamisha umma kuhusu kuahirishwa kwa kikao cha kushirikisha umma,” ilisema taarifa hiyo.
Bila kutoa maelezo zaidi, taarifa hiyo ilimalizia kwamba kikao hicho kilichokuwa kimepangwa kuandaliwa Otoba 5, 2016 katika ukumbi wa SHA, hakitafantika hadi pale ambapo mahakama itatoa maelekezo zaidi.
Lengo la KECOBO la kuandaa kikao hicho ni kupima ufaafu wa mashirika sita yanayotafuta leseni za kufanya kazi kama Mashirika ya Usimamizi wa Pamoja wa Hakimiliki, CMOs.
Taasisi hiyo imesema wahusika wanaovutiwa wanaweza kutoa maoni kuhusu waombaji hao kwa mujibu wa Kanuni ya 11(2)(c) ya Kanuni za Hakimiliki (Usimamizi wa Pamoja), 2020.
Waombaji hao sita ni Music Copyright Society of Kenya, MCSK, Film Makers Rights Achievers of Kenya, FRAK, KAMP, Boralways Limited, Performing and Audio-Visual Rights Society of Kenya, PAVRISK na Collective Management Services Ltd.
Mashirika hayo yameomba kusimamia aina mbalimbali za hakimiliki, zikiwemo za kazi za muziki, kazi za sauti na picha, rekodi za sauti, haki za waandishi, wasanii, wachapishaji na haki nyingine zinazohusiana.