Kiongozi wa chama cha Orange Democratic Movement (ODM) Oburu Oginga, ameunga mkono ujenzi wa kiwanda cha kusafisha mafuta cha Dangote kitakachogharimu shilingi trilioni 2.2, akisema kitabadilisha Lamu kuwa kitovu cha viwanda na nishati.
Kupitia kwenye taarifa, Oburu alisema mradi huo utatoa nafasi za ajira 60,000, huku ukitoa ujuzi wa kiufundi na fursa tele kwa vijana wa Lamu na kaunti jirani.
Oburu alidokeza kuwa kiwanda hicho ambacho kitazalisha mapipa 700,000 za mafuta kila siku, pia kitazalisha megawati 1,000 za umeme, huku megawati 500 zikiunganishwa kwenye mfumo wa kitaifa wa usambazaji umeme.
“Mradi huu utaimarisha usambazaji wa nishati katika eneo la pwani, wafanyabiashara wa eneo hilo na kusitisha kupotea kwa nguvu za umeme,” alisema Oburu.
Kulingana na Oburu, kiwanda hicho kitachochea ukuaji wa viwanda kama vile za uzalishaji bidhaa, kemikali na upakiaji.
Oburu, alipongeza hatua ya Rais William Ruto ya kuunga mkono mradi huo, akisema utawala wa Ruto uliondoa vikwazo vilivyodumaza utekelezaji wake.
Hata hivyo, alitoa wito kwa serikali na wawekezaji kuhakikisha wakazi watakaoathiriwa na ujenzi wa kiwanda hicho wanafidiwa.