Uzeni sera sasa, tumechoka na ‘wantam’, upinzani waambiwa

Rais Ruto anasema upinzani unapaswa kuwaelezea Wakenya utakavyotoa huduma muhimu kama vile usambazaji wa maji na umeme badala ya kutilia maanani tu kaulimbiu.

Martin Mwanje
1 Min Read
Rais William Ruto wakati wa ziara yake katika kaunti ya Kajiado

Upinzani umetakiwa kukoma kuwachosha Wakenya na kaulimbiu za kila mara zisizokuwa na maana za Kasongo na “wantam”. 

Rais William Ruto amesema wakati umewadia kwa wapinzani wake kuwaambia Wakenya watakachowafanyia ikiwa wataingia madarakani.

“Lakini mimi nataka niwaeleze wale majamaa. Tumesikia hiyo yenu ya wantam, tumesikia ya Kasongo. Sasa muwache kutupigia makelele, mtuambie sera yenu ni gani? Mtuambie mipango yenu ni gani? Mtuambie ajenda yenu ni gani?” Rais Ruto aliurushia upinzani changamoto wakati akiendeleza ziara yake katika kaunti ya Kajiado leo Jumatatu.

“Si tunataka kujua watoto watasoma namna gani? Barabara itajengwa namna gani? Maji itafika namna gani? Matibabu itafika namna gani? Stima itaunganishwa namna gani?”

Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Rais Ruto kadhalika aliwataka Wakenya kukatalia mbali ukabila na siasa za migawanyiko wakati nchi ikiajiandaa kwa uchaguzi mkuu wa mwaka 2027.

“Sharti tukatae ukabila na aina zote za siasa za migawanyiko ambazo zinaathiri ajenda yetu ya maendeleo ya taifa,” alisema kiongozi wa nchi.

“Tutaendelea kufanya kazi kuelekea Kenya moja ambako kila mwananchi na kila jamii ana fursa sawa ya kunufaika kutokana na maendeleo ya taifa letu.”

 

Share This Article