Mshukiwa wa ulanguzi wa mihadarati akamatwa JKIA

Kulingana na polisi, mshukiwa huyo Jane Waithera Wateri, ambaye amekuwa akitafutwa na polisi tangu mwaka 2025, alikuwa akijaribu kusafirisha dawa hizo za kulevya kuelekea nchini Bangladesh.

Tom Mathinji
1 Min Read
Mshukiwa wa ulanguzi wa mihadarati akamatwa JKIA.

Maafisa wa Polisi wamemkamata mwanamke akijaribu kusafirisha mihadarati kupitia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta (JKIA), yenye thamani ya shilingi milioni 13.53.

Kwa mujibu wa polisi, mshukiwa huyo Jane Waithera Wateri, ambaye amekuwa akitafutwa na polisi tangu mwaka 2025, alikuwa akilenga kusafirisha dawa hizo za kulevya kuelekea nchini Bangladesh.

Kulingana na Idara ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Wateri alikuwa akielekea kuabiri ndege aliposimamishwa na baada ya kufanyiwa upekuzi, alipatikana na mihadarati hiyo.

“Uchunguzi wa awali ulibainisha kuwa mihadarati hiyo ilikuwa cocaine yenye uzani wa gramu 3383, ambayo ni ya thamani ya shilingi milioni 13,530,720,” ilisema DCI kwenye ukurasa wa X.

Mshukiwa huyo kwa sasa anazuiliwa katika kituo cha polisi cha JKIA, huku wakiendeleza uchunguzi kutambua mtandao wa ulanguzi wa mihadarati unaohusishwa na mshukiwa huyo.

Mkuu wa Idara ya Upelelezi katika Viwanja vya Ndege B. Kanyai, alisema kwa ushrikiano na asasi zingine, idara hiyo imejitolea kuhakikisha viwanja vya ndege vya Kenya havitatumika kwenye ulanguzi wa mihadarati.

TAGGED:
Share This Article