Maandalizi ya Sikuu ya Mashunjaa yanaendelea vema chini ya mwezi mmoja kabla ya sherehe za siku hiyo kuandaliwa katika kaunti tatu kwa mara ya kwanza.
Sherehe hizo ambazo huandaliwa kila Oktoba 20 zitafanyika katika kaunti za Elgeyo Marakwet, Nandi na Uasin Gishu mwaka huu.
Sherehe kuu za kuadhimisha siku hiyo zitaandaliwa katika uwanja wa Kipchoge Keino wenye uwezo wa kuwatoshea watu 15,043 huku ukarabati wake ukiwa umefikia asilimia 68.

Akizungumza wakati wa ukaguzi wa matayarisho yanayofanywa kabla ya kuandaliwa kwa sherehe za Sikukuu ya Mashujaa, Katibu katika Wizara ya Usalama wa Taifa Dkt. Raymond Omollo amesema kazi pia zinaendelea za kuboresha barabara katika miji ya Eldoret, Kapsabet na Iten.
Uunganishaji wa maji na miundombinu mingine pia itaboreshwa kuelekea sherehe hizo.
“Kama mwenyekiti wa Kamati Simamizi, nina imani kwamba tutakuwa tayari kwa sherehe hizo. Bado kuna kazi nyingi kiasi ya kufanywa, na ningependa kuishukuru kamati ya kiufundi, ambayo imefanya kazi kwa bidii ya mchwa, mara nyingi hadi usiku, ili kutufikisha umbali huu,” alisema Dkt. Omollo.

Alizipongeza serikali za kaunti za Elgeyo Marakwet, Nandi na Uasin Gishu kwa msaada wao endelevu na kuwashukuru viongozi wa eneo hilo kwa ushirikiano wao katika kufanikisha sherehe hizo.