Kamati ya Bunge la Seneti kuhusu Mshikamano wa Taifa, Fursa Sawa na Utangamano wa Kikanda imetoa wito wa kubuniwa kwa mifumo ya amani ya nyanjani, ujumuishaji vijana na kukabiliana mapema na semi za chuki mtandaoni.
Wito huo umetolewa takriban mwaka mmoja kabla ya taifa hili kuelekea kwenye uchaguzi mkuu mwaka ujao,
Kwenye mkutano na Tume ya Mshikanao na Utangamano wa Kitaifa (NCIC), maafisa wa serikali, viongozi wa mashirika ya kijamii na wananchi katika kaunti ya Kilifi leo Jumanne, kamati hiyo ilisema ipo haja ya kuchukuliwa hatua za mapema haraka iwezekanavyo badala ya kusubiri wakati kampeni za kisiasa zimeshika kasi.
Mwenyekiti wa kamati hiyo Mohamed Said Chute ambaye ni Seneta wa Marsabit, alisema mifumo ya hatua za mapema, ujumuishaji vijana na kuzuia mizozo, inapaswa kuwa imenza kutekelezwa kufikia sasa.
“Hatuwezi subiri hadi wakati kampeni za kisiasa zimeshika kasi, ndio tuanze kuzungumza kuhusu amani. Mifumo ya onyo za mapema, ushirikishaji vijana na hatua za mapema dhidi ya semi za chuki, zinapaswa kuwa zikitekelezwa nayo jamii inapaswa kuwa sehemu ya suluhisho hizo,” alisema Chute.

Akizungumza kwenye mkutano huo, mwenyekiti wa NCIC Dkt. Kepha Nyamweya Omae, alisema tume hiyo inatekeleza mpango kwa jina Salama 2027, unaolenga kujenga upya imani ya umma, ushirikiano wa asasi za serikali, ushirikishaji vijana na mfumo imara wa ufuatiliaji semi za chuki.
“Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2027, unapaswa kuchukuliwa kama mchakato na wala sio tukio la siku moja. Tunapaswa kujenga upya imani, kuwahusisha vijana na kutambua taharuki mapema kabla ya hazijageuka kuwa ghasia,” alisema Omae.
Rais wa vijana kwenye kaunti ya Kilifi, alisema vijana ni sharti wajumuishwe kwenye meza za maamuzi kuhusu upatikanaji wa amani.
Seneta Chute alikuwa ameandamana na naibu mwenyekiti wa kamati hiyo Seneta James Lomenen na wanachama wa kamati hiyo Maseneta Consolata Wakwabubi na Okiya Omtata.
Bunge la Senate linaandaa vikao vyake pamoja na vikao vya kamati katika kaunti ya Kilifi almaarufu Senate Mashinani.