Ujenzi wa kiwanda cha kusafisha mafuta Lamu kuanza Septemba 30

Naibu Rais Prof. Kithure Kindiki anasema kiwanda hicho kitasaidia kubuni takriban nafasi 50,000 za ajira na kuchochea ukuaji wa uchumi.

Martin Mwanje
1 Min Read
Picha kwa hisani ya Pumps Africa

Ujenzi wa kiwanda cha kusafisha mafuta cha East African Refinery katika kaunti ya Lamu utaanza  Jumatano, Septemba 30 wiki ijayo. 

Naibu Rais Prof. Kithure Kindiki anasema ujenzi wa kiwanda hicho ni mradi wa kupigiwa mfano utakaofungua uchumi wa eneo la Lamu na Pwani kwa jumla kwa kubuni takriban nafasi za ajira 50,000.

Aidha, Prof. Kindiki amesema mradi huo utapiga jeki jitihada za Kenya za kuwa nchi iliyostawi zaidi kiviwanda.

“Huu ni mradi muhimu zaidi kwa nchi yetu na kwa kanda hii. Unaenda kutoa huduma za petrokemikali na shughuli za kiviwanda katika eneo hili,” alisema Prof. Kindiki.

Aliyasema hayo wakati wa mkutano wa maandalizi ya mwisho ya uzinduzi wa ujenzi wa kiwanda hicho uliofanyika mtaani Karen jijini Nairobi.

Rais William Ruto anatarajiwa kuongoza uzinduzi wa kiwanda hicho kwa kuweka jiwe la msingi huku Marais kadhaa wa kanda ya Afrika Mashariki wakitarajiwa kuhudhuria hafla hiyo.

Kiwanda hicho kinatarajiwa kujengwa na bilionea wa Nigeria Aliko Dangote aliyekutana na Rais Ruto jana Jumatatu pembezoni mwa mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, UNGA jijini New York nchini Marekani.

 

 

 

Share This Article