Gavana wa kaunti ya Kwale Fatuma Achani amekariri kujitolea kwa serikali yake kuboresha utoaji wa huduma bora za afya.
Achani, alidokeza kuwa Wizara ya Afya kwenye kaunti hiyo, imetengewa kitita cha shilingi milioni 149 katika mwaka wa fedha 2026/2027 kuwaajiri maafisa wa afya wa vitengo mbalimbali kushughulikia uhaba wa wahudumu hao.
Aidha, Gavana huyo alithibitisha kwamba, serikali yake imenunua na kuanza kutumia vifaa vya kutoa matibabu ya kitaalam ambavyo ni pamoja na mashine za CT scan, mashine ya Ultrasound, vifaa vya uchunguzi kwenye maabara na vile vya upasuaji katika hopsitali ya Rufaa na Mafunzo ya Msambweni Level 5, hospitali za Level 4 na zile za Level 3.
Kuhusu idadi ya magari ya kuwabeba wagonjwa, Achani aliyefika mbele ya Kamati ya Bunge la Seneti kuhusu Afya ambayo iliandaa vikao vyake katika kaunti ya Kilifi, alisema kaunti hiyo kwa sasa ina magari 15 ya kuwabeba wagonjwa huku madereva wa magari hayo wakipokea mafunzo kuhusu utayari wa dharura.
Wakati huo huo, alisema kituo cha matibabu ya ugonjwa wa saratani kwenye hospitali ya kaunti ndogo ya Kwale sasa kinatoa huduma kikamilifu baada ya kufanyiwa ukaguzi na idara mbalimbali.
Vikao vya Bunge la Seneti vinaandaliwa katika kaunti ya Kilifi almaarufu Senate Mashinani, Maseneta wakiandaa vikao kwa kamati na kuzuru taasisi mbalimbali kwa ukaguzi.